UNICEF yamteua Rais Kenyatta wa Kenya kuwa mtetezi wa uwezeshaji vijana duniani
-
Mkurugenzi wa UNICEF Henrietta Fore na Rais Uhuru Kenyatta, Ikulu ya Nairobi,
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amekubali ombi la Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto UNICEF, la kumteua kuwa mtetezi wa uwezeshaji vijana duniani.
Rais Kenyatta alikubali ombi hilo Ijumaa wakati alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Bi. Henrietta Fore aliyemtembela katika Ikulu ya Nairobi.
Bi. Fore amesema Rais Kenyatta atakuwa na jukumu la kutetea masuala ya afya, elimu na lishe miongoni mwa vijana kote duniani.
Mkuu huyo wa UNICEF amesema ataisaidia Kenya katika kufikia lengo lake la huduma za afya kwa wote pasina kuwepo gharama za juu.
Huduma za afya kwa wote ni kati ya nguzo nne ambazo Rais Kenyatta ametangaza kuzingatia katika muhula wa pili wa utawala wake zingine zikiwa ni usalama wa chakula, ujenzi wa makazi na ustawi wa viwanda.
Bi. Fore amempongeza Rais Kenyatta kwa nguzo zake hizo nne za utawala na kuzitaja kuwa muhimu katika kuifanya Kenya kuwa kigezo katika eneo hasa katika utoaji huduma za afya kwa watoto. Aidha amesema UNICEF itaisaidia serikali ya Kenya kuhakikisha kuwa mpango huo unatekelezwa kwa mafanikio.