Polisi Kongo DR yajiweka tayari kuzima maandamano dhidi ya Kabila
Maafisa wa polisi wameonekana wakilinda doria katika kila kona ya mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, masaa machache kabla ya kuanza maandamano ya kumshinikizi Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo aachie ngazi.
Viongozi wa Kanisa Katoliki nchini humo wamewataka wananchi kushiriki kwa wingi katika maandamano ya amani ya kutaka kutamatishwa miaka 17 ya utawala wa Kabila.
Wiki tatu zilizopita, maandamano mengine kama ya leo yaliitishwa na wakuu wa Kanisa Katoliki, ambapo polisi walikabiliana na waandamanaji na kuua na kujeruhi kadhaa miongoni mwao.
Maandamano ya leo yanatazamiwa kuwa makubwa zaidi kwa kuwa yamepigwa jeki na Jumuiya ya Waislamu nchini Kongo.
Sheikh Ali Mwinyi M'Kuu, mwakilishi wa masuala ya sheria wa jumuiya hiyo ameitaka serikali kuruhusu maandamano ya amani kufanyika akisisitiza kuwa, iwapo maafisa usalama watatumia nguvu kuyazima, basi amani haitashuhudiwa.
Itakumbukwa kuwa, watu 12 waliuawa, makumi ya wengine kujeruhiwa mbali na mamia kutiwa nguvuni, katika maandamano ya Disemba 31 mwaka jana dhidi ya utawala wa Rais Kabila.