UNICEF yataka watoto wa DRC wasaidiwe haraka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39707-unicef_yataka_watoto_wa_drc_wasaidiwe_haraka
Mjumbe wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (Unicef) huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameyataka mataifa ya dunia kukusanya dola milioni 268 za kudhamini mahitaji ya dharura ya watoto milioni 6 na laki tatu wa nchi hiyo.
(last modified 2025-11-19T02:13:06+00:00 )
Jan 31, 2018 04:31 UTC
  • UNICEF yataka watoto wa DRC wasaidiwe haraka

Mjumbe wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (Unicef) huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameyataka mataifa ya dunia kukusanya dola milioni 268 za kudhamini mahitaji ya dharura ya watoto milioni 6 na laki tatu wa nchi hiyo.

Mjumbe huyo, Dk Tajudeen Oyewale ametahadharisha kuwa, iwapo jamii ya kimataifa haitachukua hatua za kweli za kuwasaidia watoto hao, basi mustakbali wao utazidi kuwa hatarini.

Amesisitiza kuwa, watoto walioathiriwa vibaya na vita wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanahitajia mno kukomeshwa machafuko na kufikishiwa huduma za afya, elimu na kujengewa mashule.

Unicef

 

Familia nyingi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinashindwa kupata hata mahitaji ya lazima kabisa ya chakula kutokana na vita vya mara kwa mara katika maeneo yao.

Machafuko hayo yamesababisha zaidi ya watu milioni nne kuwa wakimbizi wakiwemo watoto wadogo milioni mbili na laki sita.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hasa maeneo yake ya mashariki yamekumbwa na machafuko na mapigano ya mfululizo kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Kushindwa jeshi la serikali na askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa kuyamaliza makundi ya waasi ni moja ya sababu kuu za kuendelea machafuko katika nchi hiyo kubwa na pana ya katikati mwa Afrika ambayo ina utajiri mkubwa wa maliasili.