Mahakama Kuu ya Kenya yaagiza kufunguliwa kwa runinga zilizokatiwa matangazo
Mahakama Kuu nchini Kenya imesimamisha agizo la serikali ya nchi hiyo la kufunga kwa muda usiojulikana urushaji wa matangazo ya vituo vitatu maarufu vya televisheni nchini humo.
Akisoma hukumu hiyo leo Alkhamisi, Jaji Chacha Mwita wa mahakama hiyo ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo kurejesha upeperushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya runinga hizo, hadi kesi kuhusu kadhia hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa Februari 14.
Stesheni binafsi za redio na televisheni za Citizen, KTN na NTV zilikatiwa matangazo yao hapo juzi baada ya kurusha hewani mubashara sherehe ya muungano wa upinzani wa NASA ya kumwapisha kinara wa upinzani Raila Odinga kuwa 'rais wa wananchi'.
Hapo jana, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo, Fred Matiang'i alisema stesheni hizo zitasalia kufungwa kwa muda usiojulikana, hadi pale serikali itakapomaliza uchunguzi wake.
Matiang'i anazituhumu baadhi ya duru katika vyombo vya habari kwa kufanya kile alichoeleza kuwa ni "kitendo haramu" cha kuhatarisha maisha ya maelfu ya Wakenya.
Katika hatua nyingine, kinara mwenza wa NASA, Kalonzo Musyoka amedondokwa na machozi alipokuwa kwenye kikao na waandishi wa habari hii leo pambizoni mwa Odinga mjini Nairobi.
Musyoka ambaye hakuwepo kwenye hafla ya kuapishwa Odinga ameonekana akilia kwa uchungu wakati ambapo Odinga alikuwa analaani 'shambulizi la guruneti' dhidi ya makazi ya Musyoka ambaye anamuuuguza mkewe.