Morocco kuimarisha ulinzi mipakani kukabiliana na magendo ya binadamu na ugaidi
Vyombo vya habari vya nchini Morocco vimetangaza kuwa, Rabat ina nia ya kuanzisha vituo 10 vipya vya kusimamia na kudhibiti maeneo ya mpakani mwa nchi hiyo na Algeria.
Magazeti ya leo ya Morocco yameandika kuwa, kamati maalumu iliyoundwa kwa ajili ya suala hilo imewataka viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo kutembelea vituo kadhaa vya usimamizi karibu na mpaka wa Algeria ili waone kwa karibu kazi zinazofanywa na vituo hivyo.
Magazeti hayo yamewanukuu maafisa wa ngazi za juu wa kamati hiyo wakisema kuwa Morocco imekusudia kuongeza idadi ya vituo vya kusimamia masuala ya mpakani ili kupambana na magendo mbalimbali yakiwemo ya wanadamu pamoja na ugaidi.
Taarifa kutoka Morocco zinasema kuwa, jeshi la nchi hiyo karibuni hivi litaanza zoezi la kuanzisha vituo vipya 10 kwa shabaha ya kupunguza wimbi la magendo na kujipenyeza magaidi katika mpaka wa nchi hiyo na Algeria.
Ikumbukwe kuwa Morocco na Algeria kila moja inamtuhumu mwenzake kuwa anahusika katika vitendo vya magendo ya mpakani.