Kipindupindu chaua watu tisa Malawi
Mripuko wa kipindupindu Malawi umeua watu tisa huku watu wengine 541 wakiambukizwa ugonjwa huo kitaifa.
Ugonjwa huo uliibuka Novemba mwaka jana katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo linalopakana na Tanzania na kuenea katika maeneo mengine ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.
Mwakilishi wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Kuhudumia Watoto, UNICEF, nchini Malawi Johannes Wedenig anasema maadamu watu wa Malawi hawabadilishi tabia ya kutumia maji yasiyo salama, basi itakuwa vigumu kudhibiti ugonjwa huo.
Ametoa wito kwa Wamalawi kuzingatia usafi akisisitiza umuhimu wa kunawa mikono kabla ya kula na kutayarisha chakula.

Kipindupindu ni ugonjwa hatari unaosababishwa na bakteria hasa katika utumbo mwembamba. Bakteria hao husababisha kuhara na kutapika sana pamoja na homa kali. Maambukizi hutokea hasa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa na wadudu kama vile nzi.
Kiwango cha kuhara na kutapika husababisha upungufu wa maji na uwiano wa chumvi mwilini. Baada ya dalili hizo kutokea kuna hatari ya kifo kwa asilimia 20 - 70 ya wagonjwa kama hawakupata tiba.
Inawezekana kujilinda na kipindupindu kwa kunywa maji safi na salama.