Serikali ya Somalia: Tumekamata wanachama 100 wa al-Shabab
Makumi ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabab wamekamatwa na vyombo vya usalama vya Somalia.
Abdulfattah Halane, Msemaji wa serikali ya mitaa ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika katika eneo la Houdan amesema wanachama zaidi ya 100 wa kundi la al-Shabab wametiwa nguvuni katika operesheni inayoendelea katika mji mkuu Mogadishu na viunga vyake.
Halane amesema polisi ya Somalia kadhalika imefanikiwa kurejesha mikononi mwake silaha zilizokuwa zimeporwa na wanamgambo hao wa kitakfiri.
Haya yanajiri katika hali ambayo, Jumapili iliyopita Jeshi la Somalia lilifanikiwa kuwaua magaidi zaidi ya 115 wa kundi hilo la kitakfiri katika jimbo la Galmudug nchini humo. Gavana wa jimbo hilo Abdikarim Hussein Guled alisema mapigano makali yalitokea siku ya Jumapili kati ya vikosi vya usalama na magaidi wa al-Shabab na kwamba baada ya kumalizika mapigano hayo, magaidi 115 waliuawa na wengine 110 kutiwa nguvuni.
Jeshi la Somalia linapambana na magaidi wa al-Shabab kwa kushirikiana na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM chenye askari 22,000 katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.