Mkutano wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki nchini Burundi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4093-mkutano_wa_nchi_za_ukanda_wa_afrika_mashariki_nchini_burundi
Mji mkuu wa Burundi Bujumbura ni mwenyeji wa mkutano wa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki ambao lengo lake ni kupanua ushirikiano wa pamoja na ustawi wa kijamii katika nchi hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 30, 2016 06:34 UTC
  • Mkutano wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki nchini Burundi

Mji mkuu wa Burundi Bujumbura ni mwenyeji wa mkutano wa ukanda wa nchi za Afrika Mashariki ambao lengo lake ni kupanua ushirikiano wa pamoja na ustawi wa kijamii katika nchi hizo.

Kongamano hilo la siku mbili lilianza Jumanne ya jana. Nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ni Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Tanzania, Eritrea, Ethiopia, Djibouti, Ushelisheli, Comorro, Somalia, Sudan Kusini na Mauritius. Akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo, Joseph Butore Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi alisema kuwa, kufanyika kikao hicho kwa kuhudhuriwa na viongozi wa kieneo, ni kufungua njia ya kuanzisha ushirikiano wa pamoja na kuleta uratibu wa kisiasa miongoni mwa nchi za eneo hilo. Makamu huyo wa pili wa Rais wa Burundi amesema kuwa, kueneza ustawi wa kijamii na kiuchumi kupitia njia ya ushirikiano wa serikali kuu, ni miongoni mwa malengo makuu ya kikao hicho. Aidha amesema kuwa, hapana shaka yoyote kwamba, kuimarishwa ushirikiano wa nchi za eneo kunaweza kuboresha juhudi za kukabiliana na umasikini na kuboresha maisha ya raia wa nchi hizo za Mashariki mwa Afrika.

Mkutano wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki unafanyika katika hali ambayo, akthari ya nchi za eneo hilo zimekabwa koo na jinamizi la migogoro mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama. Filihali nchi za Somalia na Kenya zinakabiliwa na ukosefu wa usalama kutokana na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab. Mapigano ya ndani katika nchi changa zaidi barani Afrika ya Sudan Kusini nayo yamewafanya maafisa wa Umoja wa Mataifa kutoa indhari mara chungu nzima juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo. Sudan Kusini inakumbwa na hali hiyo, licha ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya pande mbili hasimu. Mvutano wa kisiasa na kushika kasi vitendo vya utumiaji mabavu na mauaji huko nchini Burundi ni jambo jingine muhimu ambalo limezishughulisha nchi za eneo hilo. Nchi hizo zina wasiwasi mkubwa wa kuibuka vita vya ndani nchini Burundi na matokeo yake kuwa na taathira mbaya kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kufanyika mkutano wa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki huko Burundi, yenyewe ni hatua inayoonesha jinsi nchi hizo zinavyouzingatia mgogoro wa nchi hiyo.

Katika upande mwingine tatizo la wakimbizi na mvutano kati ya Burundi la Rwanda ni tatizo jingine katika uwanja huo. Kutokea tukio la kimaumbile la Elnino ambalo lilifuatiwa na ukame mkubwa katika baadhi ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na vile vile mvua zilizoambatana na mafuriko kulizifanya nchi nyingi zipoteze sehemu kubwa ya mazao yake. Nchi kama Ethiopia, Zimbabwe na Somalia zinakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula na viongozi wa nchi hizo wanatahadharisha juu ya kutokea ukame. Nchi za ukanda wa Afrika Mashariki zinakabiliwa na migogoro kutokana na sababu mbalimbali kama vile kupenda jaha na madaraka baadhi ya viongozi, kung'ang'ania madarakani, muundo dhaifu wa uongozi na udikteta wa watawala, kutokuweko uthabiti wa kisiasa, kubakia nyuma kiuchumi, kutokuweko usawa wa kijamii na vile vile uingiliaji wa baadhi ya madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi hizo.

Hapana shaka kuwa, kikao cha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki huko Burundi kinapaswa kutathmini mwenendo wa ustawi wa kisiasa, kuzingatia demokrasia na matakwa ya wananchi katika uga wa kisiasa; na wakati huo huo kufanya marekebisho katika sekta ya uchumi na kuvutia wawekezaji katika fremu ya ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kusaidia kuleta uthabiti katika mwenendo wa amani katika eneo hilo na hatimaye kutatua matatizo yanayozikabili nchi hizo.