Watu saba waghariki Ziwa Albert wakikimbia mapigano DRC
Kwa akali watu saba wamekufa maji wakikimbia mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, Wakongomani hao waliokuwa na nia ya kukimbilia Uganda waliaga dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama katika Ziwa Albert.
Deogratias Abaingi Rusoke, Mkuu wa Wilaya ya Kasenyi magharibi mwa Uganda amenukuliwa na AFP akisema kuwa, mtumbwi huo dhaifu ulilemewa na mawimbi ya Ziwa Albert na ndiposa ukazama, na kwamba kufikia sasa timu za uokoaji zimeweza kuopoa mwili mmoja tu.
Haya yanajiri katika hali ambayo, Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imetangaza kuwa, hadi sasa zaidi ya watu laki tatu wamekimbia makazi yao katika mkoa wa Ituri mashariki wa Kongom DR, kutokana na machafuko na ukosefu wa amani.
Ripoti hiyo inasema kuwa, idadi ya wakimbizi inaongezeka kila siku katika eneo hilo hasa kwa kuzingtia kwamba, ni vigumu kufika katika baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na machafuko.