Russia kuijengea Sudan kinu cha nyuklia cha kuzalisha umeme
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41497-russia_kuijengea_sudan_kinu_cha_nyuklia_cha_kuzalisha_umeme
Waziri wa Maji na Umeme wa Sudan amesema nchi hiyo na Russia zimefikia makubaliano ambapo Moscow itaijengea Khartoum kinu cha nyuklia cha kiwango cha chini kwa ajili ya kuzalisha umeme.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2018 04:31 UTC
  • Russia kuijengea Sudan kinu cha nyuklia cha kuzalisha umeme

Waziri wa Maji na Umeme wa Sudan amesema nchi hiyo na Russia zimefikia makubaliano ambapo Moscow itaijengea Khartoum kinu cha nyuklia cha kiwango cha chini kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Mu'taz Musa ameongeza kuwa mbali na hayo, Sudan ina mpango wa kujenga kinu kikubwa cha nishati ya nyuklia katika kipindi cha miaka minane ijayo chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

Waziri wa Maji na Umeme wa Sudan amebainisha kuwa wizara yake inakusudia kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme na kuleta uthabiti katika usambazaji nishati hiyo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Sudan imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa nishati ya umeme kutokana na miundombinu mibovu katika sekta hiyo.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita umeme ulizimwa mara tatu kwenye maeneo yote ya nchi hiyo.

Rais Omar Al Bashir wa Sudan (kushoto) na Rais Vladmir Putin wa Russia walipokutana mjini Sochi, Russia

Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana, Russia na Sudan zilisaini mkataba wa ushirikiano katika sekta ya nishati ya nyuklia wakati wa safari ya Rais Omar Al Bashir wa Sudan nchini Russia.

Shirika la Nishati ya Atomiki la Russia Rosatom lilitoa taarifa wakati wa safari hiyo ya al Bashir kwamba makubaliano hayo ya nyuklia yaliyosainiwa na pande mbili yatandaa mazingira ya kuwepo ushirikiano maalumu hususan katika ujenzi wa miundomsingi ya nyuklia, utoaji mafunzo kwa wataalamu, kuanzisha vituo vya sayansi na teknolojia ya nyukllia na kujenga kinu cha nyuklia ndani ya ardhi ya Sudan.../