Kinara wa upinzani DRC azindua azma ya kuwania urais akiwa uhamishoni
Moise Katumbi, kiongozi mashuhuri wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliyeko uhamishoni amezindua rasmi azma yake ya kugombea urais katika uchaguzi ujao baadaye mwaka huu.
Sambamba na kuzindua chama kipya cha Pamoja kwa ajili ya Mabadiliko (Together for Change) atakachokitumia kuwania urais Disemba mwaka huu, Katumbi amewaambia wafuasi wake mjini Johannesburg kuwa, "Tutapambana kutwaa madaraka na naamini kuwa tutashinda vita hivi."
Hata hivyo Meya huyo wa zamani wa Katanga ambaye serikali inamtuhumu kuhusika katika kusajili mamluki wa kigeni wakiwemo askari kadhaa wa Kimarekani waliostaafu kwa lengo la kutekeleza njama dhidi ya taifa, hajaeleza ni jinsi gani anapanga kurejea nyumbani.
Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likimshinikiza Rais Joseph Kabila aruhusu kurejea nchini Moise Katumbi, ambaye serikali ya DRC ilisema itamtia mbaroni mara tu atakapotia guu nchini humo.
Mapema mwezi huu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika mahojiano na shirika la habari la Reuters, Bruno Tshibala alisema uchaguzi wa rais utafanyika Disemba 23 akisisitiza kuwa vyombo husika vipo mbioni kuhakikisha kuwa matayarisho ya zoezi hilo la kidemokrasia yanakamilika kabla ya tarehe hiyo.
Viongozi wa upinzani na wa kidini nchini Kongo DR wamekuwa wakiwataka wananchi washiriki kwa wingi katika maandamano ya amani ya kutaka kutamatishwa miaka 17 ya utawala wa Rais Joseph Kabila.