Mar 21, 2018 14:09 UTC
  • Boko Haram yawaachia huru mabinti 100 iliowateka, yaonya

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limewaachia huru mabinti 100 kati ya 110 iliowateka nyara mwezi uliopita wa Februari, kaskazini mashariki mwa nchi.

Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, genge hilo limewaachia huru wasichana hao mapema leo katika mji wa Dapchi, na kutoa onyo kali kwa wazazi watakaowapeleka mabinti zao shuleni.

Ba’ana Musa, mmoja wa mashuhuda katika mji wa Dapchi amesema wanachama hao wa Boko Haram wamesikika wakisema, "Tumewaachia wanafunzi hawa kwa huruma, lakini hili ni onyo kwa yeyote atakayempeleka mtoto wake shuleni."

Wasichana walioachiwa huru wamesema wenzao watano waliuawa na magaidi hao huku mmoja akiendelea kushikiliwa mateka. Lai Mohammed, Waziri Habari wa Nigeria amesisitiza kuwa, magaidi hao hawajalipwa kikomboleo ili kuwaachia huru wasichana hao, lakini walitoa sharti kuwa watawaachia huru pasina uwepo wa wanajeshi.

Wasichana waliotekwa na Boko Haram mjini Chibok

Haya yanajiri katika hali ambayo, hapo jana Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International  lilisema kuwa jeshi na polisi ya Nigeria ilipewa tahadhari masaa kadhaa kabla ya kufanyika shambulizi la Februari 19 lililopelekea kutekwa nyara wasichana hao 110 wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya serikali mjini Dapchi, kaskazini mashariki mwa nchi.

Sio vibaya kukumbusha hapa kuwa, Aprili mwaka 2014 wapiganaji wa Boko Haram walishambulia shule ya wasichana ya Chibok na kuwateka nyara wasichana 276 na hadi sasa hatima ya zaidi ya mia moja kati yao haijulikani.      

Tags