Watu watano wauawa kwa mripuko wa bomu katika uwanja wa mpira Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43028-watu_watano_wauawa_kwa_mripuko_wa_bomu_katika_uwanja_wa_mpira_somalia
Kwa akali watu watano wameuawa katika shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu ulilotokea katika uwanja wa mpira wa miguu, kusini mwa Somalia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 13, 2018 04:42 UTC
  • Watu watano wauawa kwa mripuko wa bomu katika uwanja wa mpira Somalia

Kwa akali watu watano wameuawa katika shambulio la kigaidi la mripuko wa bomu ulilotokea katika uwanja wa mpira wa miguu, kusini mwa Somalia.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi ya nchi hiyo imesema kuwa, mripuko huo ulitokea katika mji wa mwambao wa Barawa, kusini magharibi mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kwamba mbali na kuua watu watano, umejeruhi wengine wanane. Tayari kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab limetangaza kuhusika na shambulizi hilo. Kundi hilo lilianzisha hujuma zake nchini Somalia mwaka 2007 kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya nchi hiyo linayoituhumu kuwa ni serikali ya kikafiri.

Magaidi wa Kiwahabi wa genge la ash-Shabab wanaohusika na mauaji nchini Somalia

Mwaka 2011 jeshi la serikali kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM, lilifanikiwa kuwafurusha wanachama wa kundi hilo mjini Mogadishu na maeneo mengine muhimu ya nchi hiyo. Hata hivyo bado magaidi hao wanaendelea kudhibiti baadhi ya maeneo ndani ya nchi hiyo huku wakihusika na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na viongozi wa serikali. Somalia ni moja ya nchi masikini zaidi na isiyo na usalama duniani.