Naibu kinara wa Boko Haram akamatwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4351-naibu_kinara_wa_boko_haram_akamatwa
Naibu kinara wa kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria amekamatwa katika oparesheni ya vikosi vya usalama nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 03, 2016 13:42 UTC
  • Naibu kinara wa Boko Haram akamatwa

Naibu kinara wa kundi la kigaidi la Boko Haram nchini Nigeria amekamatwa katika oparesheni ya vikosi vya usalama nchini humo.

Kaimu msemaji wa Jeshi la Nigeria Brigadier General Rabe Abubakar amesema kuwa Khalid Albarnawi, naibu wa Abubakar Shekau kiongozi wa magaidi wa Boko Haram alikamatwa Ijumaa katika oparesheni iliyofanyika katika mji wa Lokoja, Jimbo la Kogi na sasa anashikiliwa katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.

Albarnawi anaaminika kupata mafunzo yake ya kijeshi nchini Algeria na ana ushawishi mkubwa katia kundi la magaidi wakufurishaji wa Boko Haram.

Wakati huo huo jeshi la Nigeria limetangaza kuwaua magaidi 9 wa Boko Haram katika eneo la Bama kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake Nigeria mwaka 2009, watu elfu 20 wamepoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.