May 12, 2018 14:09 UTC
  • Watu kadhaa wauawa na kujeruhiwa katika mapigano mapya kusini mwa Libya

Watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano mapya yaliyotokea katika mji wa Sabha, kusini magharibi mwa Libya.

Ali Busibiheh, Mkuu wa Baraza Kuu la Kikabila nchini Libya amesema kuwa, mapigano hayo mapya yaliibuka asubuhi ya leo kati ya askari wa kikosi cha sita cha jeshi la nchi hiyo na wapiganaji wa kabila la Toubou eneo hilo. Kwa mujibu wa Ali Busibiheh hadi sasa mapigano hayo bado yanaendelea kati ya pande mbili. Hata hivyo Mkuu wa Baraza Kuu la Kikabila nchini Libya hakutaja idadi kamili ya uharibifu na maafa yaliyosababishwa na mapigano hayo.

Wapiganaji wa kabila la Toubou mjini Sabha, Libya

Tangu mwezi Februari mwaka huu, mji wa Sabha umekuwa ukikumbwa na mapigano ya hapa na pale ya kikabila ambapo kwa mujibu wa ripoti za kitabibu, makumi ya watu wameuawa na kujeruhiwa. Aidha mapigano hayo yamezifanya mamia ya familia kuwa wakimbizi. Kwa mara kadhaa Umoja wa Mataifa sambamba na kutahadharisha juu ya wasi wasi wake kutokana na kushtadi mapigano ya wabeba silaha mjini hapo, umetaka kukomeshwa utumiaji nguvu katika maeneo yenye watu wengi, suala ambalo hata hivyo bado halijafikia tamati.

Tags