Msafara wa magari ya jeshi washambuliwa Somalia, 12 waripotiwa kuuawa
(last modified Tue, 22 May 2018 13:45:52 GMT )
May 22, 2018 13:45 UTC
  • Msafara wa magari ya jeshi washambuliwa Somalia, 12 waripotiwa kuuawa

Kwa akali askari 12 wa Jeshi la Somalia wameripotiwa kuuawa katika shambulio la bomu lililolenga msafara wa magari ya jeshi hilo katika wilaya ya Wanaweyn, yapata kilomita 30 kaskazini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu.

Genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya leo Jumanne na kusema kuwa, gaidi wa kujitoa muhanga aliliendesha kwa kasi gari lililokuwa limesheheni mabomu na kuligongesha kwenye magari ya jeshi la Somalia yaliyokuwa yakitoka eneo la Ballidogle yakielekea mjini Mogadishu.

Kundi hilo la kigaidi limedai kwamba shambulizi hilo la bomu limelenga msafara wa magari yaliyokuwa yamewabeba askari ambao wamepewa mafunzo ya kijeshi na Marekani.

Hata hivyo jeshi la Somalia halijatoa taarifa yoyote ya kuthibitisha kutokea shambulizi hilo na idadi ya wahanga. 

Wanachama wa al-Shabaab

Haya yanajiri siku chache baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kurefusha muda wa kazi za Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia Amosom, hadi tarehe 31 Julai mwaka huu.

Kazi za kikosi cha Amisom zilianza mwaka 2007 huko Somalia kwa ajili ya kuisaidia serikali dhaifu iliyokuwa inaungwa mkono kimataifa kupambana na genge la kigaidi la al-Shabaab.

 

Tags