FAO yasema vyama vya ushirika vinaweza kuimarisha kilimo Afrika
Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa FAO linasema sekta ya ukulima Afrika inaweza kustawishwa zaidi iwapo mkulima wa kijijni naye atajengewa uwezo kupitia vyama vya ushirika.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva amesema hayo huko Utretch nchini Uholanzi wakati wa mkutano wa tatu wa kimataifa kuhusu chakula kwanza, kipaumbele kikipatiwa ujasiriamali kwenye kilimo au kilimo biashara.
Amesema sera bora inatakiwa barani Afrika lakini hiyo pekee haitoshi kwani lazima kuimarishwa vyama vya ushirika ambavyo ndivyo mkombozi wa mkulima mashinani.
Da Silva amesema bila hivyo, watakaonufaika na kilimo cha kibiashara watakuwa wakulima wakubwa ambao wanashikilia mchakato mzima wa chakula kuanzia kilimo mashambani hadi sokoni.
Inakadiriwa kuwa kilimo barani Afrika kinatarajiwa kuchangia dola trilioni moja ifikapo mwaka 2030.
Kwa msingi huo FAO imesema ili wakulima wadogo wasibakie nyuma katika kunufaika na fursa hiyo, vyama vya ushirika ambavyo kwavyo mkulima anaweza kupata sauti, ni lazima viangaziwe na kujengewa uwezo ili uzalishaji uwe wa kisasa na uendane na mahitaji ya soko.
Ili kufuatilia kivitendo suala hilo, FAO inashirikiana na taasisi ya Rabbobank ili kusaidia wakulima wadogo na vyama vya ushirika kwenye nchi zinazoendelea waweze kujitegemea kiuchumi.
Tayari nchini Tanzania, wabia hao wamesaidia wakulima wa mpunga na mihogo kuwa na mbinu bunifu za umwagiliaji na uhifadhi wa mazao.