Mwanasiasa Mauritania: Imamu Khomeini (MA) ameiokoa Quds kutokana na kusahaulika
Mkuu wa Chama cha Democratwi Wahdawi nchini Mauritania amesema kuwa, Ubunifu wa Imamu Khomeini (MA) katika kuitaja Ijumaa ya mwisho ya mwezi wa Ramadhani kuwa siku ya Kimataifa ya Quds, kwa mara nyingine umehuisha matukufu ya Palestina kwa Waislamu duniani.
Mahfouz Ould Aziz ameyasema hayo katika mahojiano na Sherika la Habari la IRNA na kuongeza kuwa, hatua ya Imamu Khomeini (MA) Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamui ya Iran katika kuiainisha Ijumaa ya mwisho ya mwezi Ramadhani kuwa siku ya Quds, ilikuwa ya kiweledi. Ameongeza kwamba, Imamu Khomeini daima alikuwa mtetezi wa watu wanaodhulumiwa duniani ambapo baada ya mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran pia alitoa amri ya kuligeuza jengo la uwakilishi wa Uzayuni kabla ya mapinduzi mjini Tehran kuwa la Wapalestina.

Mahfouz Ould Aziz amesisitiza kwamba, mwasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisimama imara katika kukabiliana na Wazayuni, ubeberu wa dunia na madhalimu wote katika kupigania haki za raia madhlumu wa Palestina. Aidha mkuu huyo wa Chama cha Democratwi Wahdawi nchini Mauritania amewataka raia wote, vyama vya kisiasa, asasi za kijamii na shakhsia mbalimbali nchini Mauritania kuyaunga mkono matukufu ya Palestina na kwamba kila mmoja anatakiwa kutumia uwezo wake wa kisiasa, kifedha, vyombo vya habari na hata kijeshi katika kuwasaidia Wapalestina. Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds yalifanyika jana katika miji 900 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika nchi mbalimbali za dunia.