Mabunge ya Iran na Kodivaa kuimarisha uhusiano baina yao
Balozi wa Iran nchini Ivory Coast ameonana na Spika wa Bunge la Senate la nchi hiyo na kujadiliana naye njia za kuimarishwa uhusiano baina ya mabunge ya nchi hizi mbili.
Mansour Shakib Mehr ameonana na Spika wa Baraza la Senate la Ivory Coast, Jeannot Ahoussou-Kouadio na pande mbili zimetilia mkazo suala la kutumia kikamilifu fursa zote zilizopo hususan katika upande wa mabunge na uhusiano wa kiuchumi na wa kibiashara baina ya Iran na Kodivaa.
Balozi Shakib Mehr amegusia uhusiano uliopo baina ya mabunge ya nchi hizi mbili ikiwa ni pamoja na kutembeleana maafisa wa mabunge mawili katika miaka ya hivi karibuni na kusisitizia umuhimu wa kushirikiana wabunge wa nchi hizi mbili.
Balozi huyo wa Iran vile vile amefikisha salamu za Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran kwa Spika huyo wa Baraza la Sanate la Ivory Coast.
Kwa upande wake, Jeannot Ahoussou-Kouadio, Spika wa Baraza la Sanate la Kodivaa ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ustaarabu wake mkongwe na maendeleo yake katika nyuga tofauti za kielimu, kiviwanda, kiufundi, kiuhandisi, kitiba na kadhalika na kuelezea hamu ya nchi yake ya kutumia uzoefu wa Iran katika nyuga zote hizo.