Watu 30 waaga dunia katika ajali ya barabarani Cameroon
Watu wasiopungua 30 wamepoteza maisha katika ajali iliyotokea katika barabara inayouunganisha mji mkuu wa Cameroon, Yaounde na mji wa Bafoussam, makao makuu ya eneo la Magharibi.
Naseri Paul Bea, Gavana wa eneo la kati amesema ajali hiyo ya jana Ijumaa ilitokea baada ya basi la abiria kupoteza muelekeo na kudondoka mtoni, katika mji wa Boutorou.
Ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba, vyombo vya dola vimeanzisha uchunguzi kubaini kiini cha ajali hiyo.
Ombang Christian, mmoja wa manasuru wa ajali hiyo amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa: "Karibu kila abiria amepoteza maisha, watu watano tu ndio walionusurika."

Ajali za namna hii hutokea mara kwa mara nchini Cameroon, akthari ya ajali hizo zikitokana na miundombinu mibovu na madereva kutokuwa waangalifu na kutoheshimu sheria za barabarani.
Mwezi Machi mwaka huu, watu watano walipoteza maisha huku wengine 20 wakijeruhiwa katika ajali nyingine ya barabarani iliyotokea karibu na eneo palipotekea ajali ya jana Ijumaa nchini Cameroon.
Kwa mujibu wa Wizara ya Uchukukuzi nchini humo, kwa wastani watu 1,500 hufariki dunia kila mwaka katika matukio ya ajali za barabarani.