Amnesty International yamjia juu Rais Magufuli kwa kuwadhalilisha wafungwa wa Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46835-amnesty_international_yamjia_juu_rais_magufuli_kwa_kuwadhalilisha_wafungwa_wa_tanzania
Shirikisha la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limemkosoa vikali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutaka wafungwa nchini humo kufanyishwa kazi usiku na mchana na kupigwa mijeledi wakiwa wavivu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 17, 2018 07:31 UTC
  • Amnesty International yamjia juu Rais Magufuli kwa kuwadhalilisha wafungwa wa Tanzania

Shirikisha la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limemkosoa vikali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutaka wafungwa nchini humo kufanyishwa kazi usiku na mchana na kupigwa mijeledi wakiwa wavivu.

Amina Hersi, afisa wa Amnesty katika kanda ya Afrika Mashariki amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema kuwa, matamshi hayo ya Rais John Magufuli ni ya kikatili na yasiyo na chembe ya utu.

Amesema, "Kauli ya Rais Magufuli ya kutaka wafungwa wavivu wapewe kichapo sio tu ni ya ukatili, bali pia iwapo agizo hilo litatekelezwa, utakuwa ni ukatili, ukosefu wa ubinadamu na kutoheshimiwa hadhi na haki za binadamu."

Mbali na Amnesty International, mashirika mengine ya kutetea haki za binadamu haswa ya nchini Tanzania yameipinga vikali kauli hiyo ya Magufuli yakisema kuwa kutekelezwa kwake ni kukiuka haki za wafungwa.

Wafungwa Tanzania

Onesmo Olengurumwa, Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini humo amesema kuwa, mfungwa licha ya kufungwa ana haki za binadamu kama kula, kuishi na kadhalika.

Naye Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini Tanzania (LHRC) amesema, ingawa Tanzania haijaridhia mkataba wa kimataifa unaopinga mateso kwa wafungwa, hiyo haitoi mwanya kwa mfungwa kuteswa.