Jul 25, 2018 01:20 UTC
  • Bemba kurejea nyumbani Kongo DR wiki ijayo kuwania urais

Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye mwezi Mei mwaka huu aliondolewa mashitaka na kuachiwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), anatazamiwa kurejea DRC wiki ijayo.

Eve Bazaiba, Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha Movement for the Liberation of Congo (MLC) chake Jean-Pierre Bemba amesema, "Bemba atarejea nyumbani Agosti Mosi, maandalizi yote yako shwari."

Amesema Bemba anarejea nchini Kongo DR kwa ajili ya kuwasilisha vyeti vyake vinavyohitajika ili aidhinishwe kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao nchini humo. Zoezi la kuwasajili wagombea wa urais linafanyika kuanzia leo Jumatano hadi Agosti 8. 

Julai 13, chama cha (MLC) kilimtangaza Jean-Pierre Bemba kuwa mgombea wake wa urais katika hafla iliyofanyika katika mji mkuu Kinshasa. Bemba ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji, muda mfupi baada ya tangazo hilo alihutubia wafuasi wake kwa njia ya simu, na kuwaahidi kuwa atarejea nyumbani karibuni hivi.

Bemba akiwasili katika mahakama ya ICC, mjini The Hague, Uholanzi

Bemba mwenye umri wa miaka 55, ambaye amekuwa katika kizuizi cha ICC tokea mwaka 2008, alipatikana na hatia ya kuhusika na jinai dhidi ya binadamu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 18 gerezani mwaka 2016, lakini aliachiwa huru hivi karibuni baada ya kukata rufaa kwenye kesi hiyo.

Uchaguzi mkuu nchini DRC unatazamiwa kufanyika Disemba 23 mwaka huu.

Tags