Rais wa Ivory Coast atoa msamaha kwa wafungwa 800 wa kisiasa
(last modified Tue, 07 Aug 2018 14:35:55 GMT )
Aug 07, 2018 14:35 UTC
  • Rais wa Ivory Coast atoa msamaha kwa wafungwa 800 wa kisiasa

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast ametangaza msamaha kwa wafungwa wapatao 800 wa kisiasa ikiwa imesalia miaka miwili kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi.

Ouattara ametangaza uamuzi huo katika hotuba aliyotoa kwa njia ya televisheni katika utaratibu wa jadi aliojiwekea sambamba na kukaribia maadhimisho ya uhuru wa Ivory Coast. Amesema amesaini msamaha huo ambao unajumuisha wafungwa wapatao 800 wakiwemo wale waliohukumiwa kwa makosa yanayohusiana na mgogoro uliozuka nchini humo baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 na yale ya masuala ya usalama yanayohusiana na kipindi cha kuingia kwake madarakani mnamo Mei 21 2011.

Katika hotuba yake hiyo, Rais wa Ivory Coast ametangaza msamaha kwa Simone Gbagbo, mke wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Laurent Gbagbo, waziri wa zamani wa ulinzi Lida Kouassi ambaye ni muitifaki mkuu wa Gbagbo na ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela mapema mwaka huu kwa kula njama na waziri wa zamani wa ujenzi Assoa Adou ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela mwaka uliopita wa 2017.

Simone Gbagbo

Rais Ouattara amesema, watu 500 kati ya hao wameshaachiliwa huru na wengine 300 wataachiwa huru hivi karibuni.

Itakumbukwa kuwa watu wapatao 3,000 waliuawa katika mji mkuu wa Ivory Coast, Abidjan katika machafuko yaliyozuka baada ya uchaguzi wa rais mwaka 2010 ambapo aliyekuwa rais wa nchi hiyo Laurent Gbagbo alikataa kushindwa na mpinzani wake, Alasane Ouattara rais wa sasa wa nchi hiyo.

Muongo mmoja wa mgogoro wa kisiasa na kijeshi ulioigawa vipande vipande Ivory Coast unatajwa kama doa jeusi kwa kipindi cha uongozi wa rais Ouattara.../