Aug 30, 2018 04:18 UTC
  • Mapigano yaanza tena katika mji mkuu wa Libya, Tripoli

Mapigano yameanza tena katika mji mkuu wa Libya Tripoli baina ya pande zinazozozana nchini humo baada ya usitishaji vita wa muda mfupi.

 Ripoti kutoka Libya zinasema kuwa, mapigano yalianza jana katika eneo la Khallet Al-Forjan mjini Tripoli na kwamba, pande mbili zinazopigana zimeshambuliana kwa silaha nzito.

Msemaji wa vikosi vya usalama mjini Tripoli amewaambia waandishi wa habari kwamba, wanamgambo wa kabila la Kani wameyashambulia baadhi ya maeneo ya Tripoli kwa silaha nzito.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, baadhi ya raia wa mji mkuu Tripoli wameonekana wakiyakimbia makazi yao baada ya kushadidi mapigano hayo.

Hadi sasa hakuna taarifa rasmi zilizotolewa kuhusiana na idadi ya watu waliouawa katika mapigano hayo yaliyozuka jana mjini Tripoli.

Libya inavyoshuhudia machafuko

Mapigano hayo yamezuka siku moja tu baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Libya Abdulsalam Ashour kutangaza siku ya Jumatatu kwamba, kumefikiwa makubaliano ya kusimamisha mapigano katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli, kufuatia mapigano makali kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wenye silaha. 

Baadhi ya duru zimeinukuu Wizara ya Afya ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ikitangaza kuwa, watu watano wameuawa katika machafuko yaliyoanza siku ya Jumatatu mjini Tripoli katika baadhi ya maeneo.

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO).

Tags