Sita wauawa katika hujuma ya kigaidi Mogadishu, Somalia
Watu wasiopungua sita wameuawa baada ya gaidi mmoja kushambulia kwa bomu ofisi ya serikali za mitaa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Hujuma hiyo imejiri Jumapili asubuhi ambapo jengo lililolengwa limeharibika kabisha na pia shule iliyokuwa karibu nayo jengo lake limeanguka. Kati ya watu watatu waliopoteza maisha katika hujuma hiyo ni maafisa wa usalama waliojaribu kumzuia gaidi ambaye gari lake lilikuwa limesheheni bomu. Gaidi huyo alilipua gari lake lililokuwa limesheheni bomu karibu na lango la makao makuu ya Wilaya ya Hawldawag. Watu wengine waliouawa katika hujuma hiyo ni raia wa kawaida huku watu wengine 14, wakiwemo watoto sita, wakijeruhiwa vibaya.

Kundi la kigaidi la al-Shabab limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo pia imeharibu paa la msikiti karibu na eneo la mlipuko. Magaidi wakufurishaji wa al-Shabab ambao aghalabu wanafungamana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wanaendesha kampeni ya mauaji kwa lengo la kuiangusha serikali ya Somalia yenye makao yake Mogadishu na ambayo inaungwa mkono na Umoja wa Mataifa.