Sep 08, 2018 15:17 UTC
  • Watu 9 wauawa katika machafuko mapya Jamhuri ya Afrika ya Kati

Msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati kinachojulikana kwa jina la MINUSCA ametangaza habari ya kuuawa watu 9 katika shambulio la kulipiza kisasi lililotokea mjini Bria, katikati mwa nchi hiyo.

Vladimir Monteiro amesema hayo leo na kuongeza kuwa, watu hao 9 walikuwa wanaishi kwenye kambi ya wakimbizi katika mji wa Bria na wameuliwa baada ya kutoka nje ya kambi hiyo. Walitekwa nyara juzi Alkhamisi na baadaye kuuawa.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa MINUSCA, kundi linalojiita Harakati ya Wananchi ya Kuifufua Upya Jamhuri ya Afrika ya Kati yalikusudia kulipiza kisasi dhidi ya genge la kigaidi la Anti-Balaka.

Msemaji huyo wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati ameyataka makundi yote kudumisha amani na utulivu kama ambavyo amelaani maandamano ya watu 400 yaliyofanyika jana Ijumaa mbele ya kituo cha MINUSCA mjini Bria. 

Magaidi wa Kikristo wa Anti Balaka

 

Machafuko yameikumbwa Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu mwaka 2013; na hadi hivi sasa mashambulizi na mapigano ya hapa na pale yanaendelea kuripotiwa licha ya kikosi cha kulinda amani ya Umoja wa Mataifa (MINUSCA) kutumwa nchini humo.

Mapigano hayo yamepelekea mamia ya watu kuuawa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi. Rais Faustin-Archange Touadéra wa nchi hiyo hadi hivi sasa ameshindwa kurejesha amani na utulivu nchini humo.

Tags