Amnesty yasajili jinai mpya za kivita nchini Sudan Kusini
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeituhumu serikali ya Sudan Kusini na makundi ya wabeba silaha yanayoungwa mkono na serikali hiyo kwamba yametenda jinai za kivita na ukatili wa kutisha dhidi ya raia.
Ripoti iliyotolewa leo Jumatano na Amnesty International imesema kuwa, shirika hilo lina ushahidi wa jinai hizo kutoka kwa raia 100 waliofanikiwa kutoroka mashambulizi ya maafisa usalama na magenge ya wabeba silaha waitifaki wa serikali ya Juba kati ya mwezi Aprili na Juni mwaka huu, katika kaunti za Leer na Mayendit jimboni Unity.
Joanne Mariner, mshauri mkuu wa masuala ya migogoro wa Amnesty amesema njia pekee ya kumaliza mzunguko wa jinai na mapigano katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ni kuwawajibisha wahusika wa pande zote, iwe ni wanajeshi wa serikali na waitifaki wao kwa upande mmoja na magenge ya upinzani kwa upande mwingine.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Haki za Binadamu ya umoja huo kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili unaofanyika Sudan Kusini inatia wasiwasi mkubwa.

Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini hivi karibuni iliashiria mateso na ukatili wa kingono unaofanyika katika nchi hiyo na kusisitiza udharura wa kushughulikiwa uhalifu uliofanyika dhidi ya raia.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani na mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya jeshi la serikali ya Rais Salva Kiir na waungaji mkono wa aliyekuwa makamu wake, Riek Machar.