Sep 24, 2018 02:57 UTC
  • Mapigano yaanza tena karibu na matangi ya mafuta huko Tripoli, Libya

Duru za kiusalama za Libya zimetangaza habari ya kuanza tena mapigano kandokando ya matangi ya mafuta huko Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo.

Mapigano hayo yameripotiwa kujiri kati ya makundi yenye silaha nzito karibu na makao makuu ya matangi ya kuhifadhia mafuta ya Shirika la al Birikha katika barabara iendayo uwanja wa ndege wa Tripoli. 

Mustafa Sanalla, Mkuu wa Shirika la Taifa la Mafuta la Libya

Mapigano hayo yamejiri huku kukiripotiwa kuvurumishwa makombora kadhaa pia kuelekea maeneo kadhaa huko Wadi al Riba kusini mwa Tripoli. Mustafa Sanallah Mkuu wa Shirika la Taifa la Mafuta la Libya siku tatu zilizopita alitahadharisha kuhusu kujitokeza tatizo la mafuta kutokana na kuharibiwa sana matangi ya kuhifadhia mafuta na kusema: Hivi sasa yamesalia matangi matatu tu ya mafuta huko Tripoli na kwamba shirika la mafuta pia linakabiliwa na matatizo ya kutuma mafuta katika mji mkuu huo kutokana na mapigano hayo.

Yapata karibu mwezi mmoja sasa tangu mji mkuu wa Tripoli uanze kushuhudia mapigano kati ya makundi yenye silaha. Tarehe tisa mwezi huu wa Septemba, makundi hayo hasimu yalisaini makubaliano ya kusimamisha mapigano kwa usuluhishi wa Umoja wa Mataifa hata hivyo makubaliano hayo hayakudumu.    

 

Tags