Sep 25, 2018 07:58 UTC
  • UN: Mapigano Libya yawaweka watoto laki 5 katika hatari kubwa

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef umetadharisha kuwa, watoto laki tano wapo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na mapigano yaliyoshtadi katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Taarifa ya Unicef imesema kuwa, mapigano hayo yamepelekea watu zaidi ya 25,000 kuyahama makazi yao, nusu ya idadi hiyo wakiwa ni watoto wadogo.

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya waliouawa katika ghasia hizo imeongezeka na kufikia watu 115, wakiwemo raia. Unicef imeripoti kuwa,  familia zaidi ya 1,200 zimelazimika kuyahama makazi yao kutokana na kushtadi mapigano hayo yaliyoanza tangu Agosti 26.

Uwanja wa ndege wa Tripoli

Hapo jana duru za kiusalama za Libya zilitangaza habari ya kuanza tena mapigano kandokando ya matangi ya mafuta ya Shirika al Birikha, katika barabara inayoelekea uwanja wa ndege wa Tripoli.

Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) mwaka 2011.

Tags