Sep 27, 2018 03:00 UTC
  • Mahasimu wakubaliana kusitisha vita vilivyoua 117 Tripoli, Libya

Makundi mawili hasimu ya waasi nchini Libya yamekubaliana kusitisha mapigano yaliyopelekea kuuawa makumi ya watu katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Serikali ya Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imesema kuwa imepokea kwa mikono miwili mapatano hayo ya usitishaji vita, kati ya makundi ya waasi ya Revolutionaries' Brigades na Nawasi Brigade yanayoiunga mkono serikali ya Tripoli.

Taarifa ya serikali hiyo imebainisha kwamba, makubaliano hayo ya kusitisha vita yamefikiwa kutokana na mazungumzo yaliyoongozwa na wawakilishi wa mji huo pamoja na viongozi wa kikabila. 

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya waliouawa katika ghasia hizo imeongezeka na kufikia watu 117, wakiwemo raia.

Kundi la waasi mjini Tripoli

Siku ya Jumanne, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa Unicef ulitadharisha kuwa, watoto laki tano wapo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na mapigano yaliyoshtadi katika mji mkuu wa Libya, Tripoli. 

Unicef imeripoti kuwa,  familia zaidi ya 1,200 zimelazimika kuyahama makazi yao kutokana na kushtadi mapigano hayo yaliyoanza tangu Agosti 26.

Tags