Sep 30, 2018 14:28 UTC
  • Cameroon: Tumelishinda na kulitokomeza kundi la Boko Haram

Rais Paul Biya wa Cameroon amesema taifa hilo limefanikiwa kuliangamiza kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram ambalo limeua maelfu ya watu na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.

Rais Biya ameyasema hayo katika ziara yake ya kwanza katika eneo la kaskazini tokea mwaka 2012, eneo ambalo limekuwa uwanja wa makabiliano baina ya maafisa usalama wa nchi hiyo na wanachama wa Boko Haram.

Akihutubia mkutano wa kampeni za kisiasa katika mji wa Maroua, Biya amesema "Tunapaswa kujishughulisha sasa na kulijenga upya eneo la Kaskazini ya Mbali lililosambaratishwa na Boko Haram, wakati huu ambapo tumeutokomeza kikamilifu ugaidi."

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanasema yumkini tangazo hilo la Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 85 na ambaye yuko madarakani kwa karibu miaka 36 sasa ni la kisiasa, kwani alikuwa akihutubia mkutano wa kisiasa kwa ajili ya uchaguzi wa rais wa Oktoba 7, ambapo anatazamiwa kugombea muhula wa saba wa miaka saba. 

Wanachama wa genge la ukufurishaji la Boko Haram

Hii ni katika hali ambayo, mwezi Julai mwaka huu, magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram walishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani ya nchi, katika eneo la mpaka wa Nigeria na Cameroon ambapo watu wasiopungua wanne waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Hadi hivi sasa zaidi ya watu 20 elfu wameshauawa katika nchi za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad kutokana na mashambulizi ya Boko Haram, huku zaidi ya milioni mbili wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.

Tags