Namibia kuwapokonya wazungu mashamba kama Afrika Kusini
Rais wa Namibia ameahidi kwamba atatwaa mashamba ya kilimo yanayomilikiwa na Wazungu nchini humo na kuyagawa kwa wananchi wazalendo wa nchi hiyo.
Akiongea katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa Kuhusu Sera ya Ardhi katika mji mkuu Windhoek, Rais Hage Geingob ametoa mwito wa kufanyiwa marekebisho katiba ya nchi hiyo ili kuipa serikali kibali cha kuwapokonya Wazungu mashamba wanayoyamiliki na kisha kuwapa raia wa nchi hiyo.
Amesema, "Nchi yetu kama vile Afrika Kusini, ina historia chungu kuhusu suala la ardhi. Na chimbuko lake ni ugawanyaji wa ardhi kwa njia zisizokuwa za kiadilifu tokea enzi za ukoloni, kamwe hatutaruhusu jambo hili kuendelea."
Namibia inatazamiwa kutwaa mashamba ya kilimo yenye ukumbwa wa hektari milioni 15 yanayomilikiwa na Wazungu na kisha kuwapa raia wazalendo wa nchi hiyo wenye kipato cha chini.
Februari mwaka huu, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, alisema serikali yake itatwaa mashamba ya wazungu bila ya kulipa fidia, ikiwa ni miongoni mwa hatua zitakazochukuliwa na serikali yake kwa ajili ya kuharakisha mchakato wa kuwarejeshea umiliki wa ardhi wazalendo wa nchi hiyo.
Wazalendo wa Afrika Kusini wanaounda asilimia 79 ya nchi hiyo wanamiliki asilimia 1.2 tu ya ardhi za kilimo nchini humo.