Afrika Kusini yatakiwa kusitisha ushirikiano wake wa kijeshi na Saudia
Wanaharakati wa masuala ya amani na haki za binadamu wa Afrika Kusini wameitaka serikali ya nchi hiyo isimamishe ushirikiano wake wa kijeshi na Saudi Arabia kutokana na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Riyadh hususan nchini Yemen.
Simnikiwe Hlatshaneni ambaye ni mwandishi na mwanaharakati wa masuala ya kiraia wa Afrika Kusini amekosoa uuzaji silaha wa serikali ya Pretoria kwa utawala wa Saudi Arabia na kusisitiza kuwa kitendo hicho kinaonesha tatizo la kimaadili kwa sababu silaha hizo zinauzwa kwa watu waovu.
Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa, Saudi Arabia inafanya mazungumzo kwa ajili ya kununua silaha kutoka Afrika Kusini na vilevile kununua kampuni ya kutengeneza silaha ya Denel inayomilikiwa na serikali ya Pretoria ambayo inasumbuliwa na matatizo ya kifedha.
Saudi Arabia inalaumiwa sana kwa kuendelea kukiuka haki za binadmu ndani ya nchi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia yoyote wa Yemen.
Saudi Arabia na washirika wake wakisaidiwa na Marekani walivamia ardhi ya Yemen Machi mwaka 2015 na wanaendelea kuizingira nchi hiyo kutokea pande zote za baharini, nchi kavu na angani.