UN yaongeza 'muda wa mwisho' wa kuhudumu kikosi chake Abyei
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepasisha azimio la kuongezewa muda wa kuhudumu kikosi chake cha kulinda amani katika eneo la Abyei, lililoko kwenye mpaka wa Sudan na Sudan Kusini.
Katika kikao cha jana Alkhamisi, baraza hilo kwa kauli moja lilipasisha azimio la kuongezewa muda wa miezi sita zaidi kikosi cha kulinda amani cha UN katika eneo la Abyei lenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Baraza la Usalama limesema hii ndio mara ya mwisho kwa kikosi hicho kuongezewa muda wa kuhudumu, huku likizitaka nchi mbili hizo jirani kuupatia ufumbuzi mgogoro wa mipaka unaozikabili.
Nchi hizo mbili zinagombaniana eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta tangu mwaka 2011, baada ya Sudan Kusini kujitenga na Sudan. Wakazi wakuu wa eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita 10,500 mraba ni watu wa kabila la Ngok Dinka la Sudan Kusini na kabila la Misseriya la Sudan.
Ugomvi uliozuka baina ya makabila hayo mawili ulipelekea majeshi ya Sudan na Sudan Kusini kuingia vitani na kusababisha vifo vya makumi ya watu na wengine wengi kukimbia makazi yao.
Vita hivyo vilipungua baada ya kutumwa zaidi ya wanajeshi elfu nne wa Ethiopia kwenda kusimamia amani katika eneo la Abyei chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa UNISFA.