Oct 15, 2018 13:54 UTC
  • Cameroon kusikiliza kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais

Tume ya Uchaguzi Cameroon Elecam imesema kesho Jumanne ndiyo siku ya kusikiliza kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni.

Baraza la Katiba nchini humo limetangaza kuwa limeshapokea mafaili 18 ya kesi hizo ambazo zitaanza kusikilizwa kuanzia kesho Jumanne Oktoba 16 katika Ukumbi wa Mikutano wa Yaounde.

Wakati huohuo, baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vimetangaza kile kinachotajwa kama matokeo yaliyovuja ya uchaguzi wa rais, yanayoonesha kuwa Rais Paul Biya ameshinda uchaguzi huo kwa zaidi ya asilimia 71 ya kura zilizopigwa.

Katika shauri lake mbele ya Baraza la Katiba nchini humi, Joshua Osih, mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha Social Democratic Front (SDF) ametaka kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi huo.

Kinara wa chama cha upinzani cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC), Maurice Kamto

Wiki iliyopita, mgombea wa urais wa chama cha upinzani cha Movement for the Rebirth of Cameroon (MRC), Maurice Kamto alijitangaza mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Oktoba 7, ingawaje Paul Atanga, Waziri wa Mambo ya Ndani nchini humo alisema Baraza la Katiba ndicho chombo pekee cha sheria chenye mamlaka ya kumtangaza mshindi wa uchaguzi huo.

Baadhi ya vyama vya upinzani viliungana siku moja kabla ya uchaguzi huo ili kupambana na Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 85 na ambaye yuko madarakani kwa karibu miaka 36 sasa. 

Tags