Oct 16, 2018 08:09 UTC
  • WHO kuunda kamati ya kujadili mlipuko wa Ebola Congo DR

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa litaitisha kikao cha kamati ya dharura ya kuamua iwapo mlipuko wa sasa wa maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni mgogoro wa umma unaoitia wasiwasi jamii ya kimataifa au la.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kuongezeka idadi ya watu walioambukizwa au kufariki dunia kutokana na virusi vya ugonjwa huo.

Kamati ya wataalamu ya WHO yumkini ikatoa mapendekezo ya jinsi ya kudhibiti mlipuko wa sasa wa ugonjwa huo uliotangazwa tarehe Mosi Agosti na unaendelea kwa kasi kubwa; suala linalotishia kuenea ugonjwa huo kutoka maeneo ya kaskazini mashariki mwa Congo hadi katika nchi jirani za Uganda na Rwanda.

Jumatatu ya jana Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alitangaza kuwa, watu 33 wamethibitishwa kupatwa na virusi vya Ebola na kwamba 24 kati yao wamefariki dunia. Kesi hizo ni zile zilizoripotiwa katika kipindi cha baina ya tarehe 8 na 14 mwezi huu wa Oktoba pekee.

Wahanga wa virusi vya Ebola, Congo DR.

Ripoti ya Wizara ya Afya ya Congo imesema kuwa, watu wasiopungua 130 wameaga dunia kutokana na virusi vya ugonjwa wa Ebola tangu mwezi Julai mwaka huu.

Wasiwasi kuhusu maambukizi ya virusi vya Ebola umeongezeka sana baada ya mfanyakazi mmoja wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuthibitishwa kwamba ameambikuzwa virusi hivyo.

Tags