UNHCR ina wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48862-unhcr_ina_wasiwasi_kuhusu_hali_ya_kibinadamu_drc
Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, lina wasiwasi na hali ya kibinadamu katika jimbo la Kasai la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na kurejea wakimbizi wengi kutoka Angola katika wiki mbili zilizopita.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 17, 2018 15:04 UTC
  • UNHCR ina wasiwasi kuhusu hali ya kibinadamu DRC

Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, lina wasiwasi na hali ya kibinadamu katika jimbo la Kasai la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutokana na kurejea wakimbizi wengi kutoka Angola katika wiki mbili zilizopita.

Maafisa wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema kuwa, wakimbizi laki mbili wamewasili katika jimbo la Kasai peke yake, na wengine wengi wanatarajiwa kuwasili katika jimbo la jirani la Kasai Kati. Kurejea kwa wakimbizi hao kunatokana na hatua ya serikali ya Angola kuamua kuwafukuza wageni wanaofanya kazi kwa njia zisizo halali kwenye machimbo ya madini. 

Ripoti zinasema kuwa, wakimbizi hao wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamerejeshwa kutoka Angola bila ya kupewa taarifa mapema.

Machafuko ya Kasai, DRC

Habari zinasema kumekuwa na mapambano katika baadhi ya maeneo ya Angola, kutokana na idara za usalama kutekeleza amri ya kuwafukuza wageni wanaoishi bila kufuata sheria, baada ya Jumatatu ambayo ilikuwa siku ya mwisho iliyowekwa na serikali kwa wageni hao kuondoka. 

Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ni kuwa, wakimbizi hao wanarejea kwa wingi katika jimbo la Kasai katika hali ambayo, jimbo hilo linakabiliwa na matatizo mengi likiwemo suala la ukosefu wa usalama.

Hivi karibuuni wakaguzi wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa walitangaza kuwa, jeshi la serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na makundi ya waasi yamefanya uhalifu unaofikia jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu ikiwa ni pamoja na kuua raia na kunajisi na kubaka wanawake na watoto katika jimbo hilo la Kasai.