Genge moja la kigaidi lasambaratishwa nchini Tunisia
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia imetangaza habari ya kusambaratishwa genge moja la kigaidi magharibi mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
Wizara hiyo imesema kuwa, askari wa kulinda usalama wa nchi hiyo wamefanikiwa kugundua na kusambaratisha genge la kigaidi lililokuwa linapanga mashambulizi ya kigaidi, katika mkoa wa el-Qaserin, magharibi mwa nchi hiyo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia aidha imesema kuwa, operesheni ya askari wa nchi hiyo imefanikiwa kumwangamiza pia kiongozi mmoja mkuu wa magaidi ambaye alikuwa katika orodha ya watu hatari sana wanaosakwa nchini humo.
Itakumbukwa kuwa wanachama wengi wa genge la kigaidi la Daesh ambao walikuwa wakifanya jinai katika nchi za Iraq na Syria walikuwa ni raia wa Tunisia. Magaidi hao wamerejea nchini kwao baada ya magaidi wa ISIS kusambaratishwa huko Iraq na Syria.

Nchi hiyo imekuwa ikishuhudia vitendo vingi vya kigaidi. Mwezi Julai mwaka huu, maafisa tisa wa polisi waliuawa katika shambulizi la kigaidi lililotokea magharibi mwa Tunisia, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Algeria.
Askari polisi hao waliuawa baada ya genge moja la kigaidi kuurushia guruneti msafara wa magari ya maafisa usalama hao, katika mji wa Gar Dimaou katika jimbo la Jendouba.
Habari zaidi zilisema kuwa, polisi hao waliviziwa na kushambuliwa na magaidi hao wakufurishaji wanaoaminika kuwa na mfugamanao na Daesh (ISIS), walipokuwa katika operesheni ya kawaida ya kulinda doria. Hiyo ilikuwa idadi kubwa zaidi ya polisi kuuawa nchini Tunisia tangu mwaka 2015, baada ya kundi la kigaidi la Daesh kuendesha wimbi la mashambulizi ya mabomu yaliyoua makumi ya maafisa usalama na watalii.