Oct 24, 2018 07:48 UTC
  • Polisi ya Guinea Conakry yatumia gesi ya kutoa machozi kukabiliana na waandamanaji

Polisi ya Guinea Conakry imetumia mabomu ya kutoa machozi kukabiliana na maandamano dhidi ya serikali ya nchi hiyo.

Conakry mji mkuu wa nchi hiyo umeshuhudia maandamano makubwa ya kuipinga serikali ambapo vyombo vya usalama vimelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.

Maandamano hayo yaliitishwa na Muungano wa Walimu pamoja na vyama vya upinzani vya nchi hiyo.

Walimu wa Guinea Conakry wanataka kuongezewa mishahara huku wapinzani wakitaka kuhesabiwa upya kura za uchaguzi wa hivi karibuni wa Mabaraza ya Miji na Umeya.

Wapinzani wa Guinea Conakry wanaamini kuwa, serikali ya nchi hiyo ilichakachua na kuiba kura katika uchaguzi huo, hivyo hawako tayari kuwatambua viongozi waliotangazwa.

Rais Alpha Conde wa Guinea Conakry

Taarifa zaidi kutoka Conakry zinasema kuwa, kijana mmoja mdogo aliuawa jana na vikosi vya usalama baada ya kutokea mapigano baina ya waandamanaji na vikosi hivyo vya usalama.

Baadhi ya asasi za kiraia zinavikosoa vyombo vya usalama vya nchi hiyo kwa kile zinachosema, vyombo hivyo vya usalama vimekuwa vikitumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na maandamano ya amani ya wananchi ambayo ni haki yao ya kikatiba.

Huku maandamano na malalamiko ya wapinzani yakiendelea kufanyika nchini humo, duru za upinzani zinasema kuwa makumi ya waandamanaji waliuawa katika maandamano ya upinzani yaliyofanyika nchini humo miaka minne iliyopita. 

Tags