Marais wawili wa zamani Madagascar waingia duru ya pili ya uchaguzi
Marais wawili wa zamani wa Madagascar, Andry Rajoelina na Marc Ravalomanana wamepata kura za kutosha katika uchaguzi wa rais ambazo zitawawezesha kuchuana katika duru ya pili mwezi ujao.
Hakuna yeyote miongoni mwao aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zinazotakiwa ili kutangazwa mshindi katika duru ya kwanza. Katika matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na tume ya uchaguzi, CENI, Jumamosi, Rajoelina alipata asilimia 39.19 ya kura huku Ravalomanana akipata asilimia 35 ya kura zote zilizopigwa. Duru ya pili ya uchaguzi huo uliofanyika Novemba 7 imepengwa kufanyika Disemba 19.
Rais wa sasa anayeondoka Hery Rajaonarimampianina aliweza kupata asilimia 8.84 tu ya kura katika uchaguzi huo ambao ulishuhudia asilimia 54.3 ya wapiga kura nchini humo wakijitokeza.
Wagombea hao watatu, ambao ni miongoni mwa wengine 36, wamedai kulikuwa na dosari kubwa katika uchaguzi na inatazamiwa kuwa matokeo ya mwisho yatapingwa mahakamani.

Hata hivyo waangalizi wa kieneo na kimataifa wanasema kulikuwa na dosari ndogo sana katika uchaguzi huo.
Mkuu wa Tume ya Uchaguzi, CENI, Hery Rakotomanana anasema wamezingatia, uwazi, kutopendelea upande wowote na uhuru katika kusimamia uchaguzi.