Watu watatu wauawa katika mripuko Somalia
Watu watatu wameuawa na wengine wasiopungua sita kujeruhiwa katika mlipuko ulitokea jana Jumatano katika soko lililokuwa na watu wengi huko Somalia.
Mripuko huo ulitokea wakati wafanyabiashara na wakulima walipokuwa wakiuza bidhaa zao katika soko la kuuzia mifugo katika wilaya ya Afgoye karibu na Mogadishu mji mkuu wa Somalia.
Abdukadir Mohamed afisa usalama wa eneo amesema kuwa watu watatu waliaga dunia na wengine sita kujeruhiwa na mlipuko huo unaotajwa kuwa huenda ulikuwa ni wa guruneti.
Hadi sasa hakuna kundi lililotangaza kuhusika na mripuko huo. Jumatatu wiki hii pia gari lililokuwa limetegwa bomu liliripuka nje ya mgahawa mmoja huko Mogadishu na kuuwa watu wasiopungua watano, wakiwemo watoto wa shule.
Somalia imekuwa ikishuhudia mashambulizi ya wanamgambo wa kundi la al Shabab tangu mwaka 2006. Magaidi hao wa kitakfiri wamekuwa wakitekeleza mashambulizi mbalimbali katika mji mkuu wa Somalia na kwingineko nchini humo, licha ya kufurushwa huko Mogadishu na katika miji mingine mikubwa na wanajeshi wa serikali na kikosi cha kulinda Amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM).