Jeshi la Rwanda laua wapiganaji wanne wa kundi la FDRL
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50098-jeshi_la_rwanda_laua_wapiganaji_wanne_wa_kundi_la_fdrl
Jeshi la Rwanda limesema askari wake wamekabiliana vikali na wapiganaji wa kundi la waasi wa FDLR waliojipenyeza nchini humo wakitokea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 11, 2018 04:42 UTC
  • Jeshi la Rwanda laua wapiganaji wanne wa kundi la FDRL

Jeshi la Rwanda limesema askari wake wamekabiliana vikali na wapiganaji wa kundi la waasi wa FDLR waliojipenyeza nchini humo wakitokea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Msemaji wa jeshi la Rwanda, Innocent Munyengango amenukuliwa na shirika la habari la  Associated Press akisema kuwa, wanachama wanne wa kundi hilo la waasi wameuawa katika mapigano hayo yaliyotokea siku ya Jumapili, magharibi mwa wilaya ya Rubavu.

Amesisitiza kuwa hakuna hata askari mmoja wa Rwanda aliyeuawa katika makabiliano hayo, lakini Meya wa Rubavu anasema raia mmoja alijeruhiwa.

Waasi wa zamani wa FDLR waliounganishwa na familia zao siku chache zilizopita

Shambulizi la mwisho kufanywa na waasi wa FDLR ilikuwa ni mwaka 2016, ambapo raia kadhaa wa Rwanda waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Miezi kadhaa iliyopita, baadhi ya waasi wa kundi la FDLR wa Rwanda walioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walijisalimisha kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliko mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi hilo liliyumba na kupata pigo mwaka 2016, baada ya askari wa serikali ya Kongo DR kumtia mbaroni kiongozi wa waasi hao, Léopold Mujyambéré kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya umati ya mwaka 1994 nchini Rwanda. 

Aidha mwaka huo huo, polisi ya Uganda ilimkamata kamanda mwingine wa FDLR anayejulikana kama Meja Barack Anan alipokuwa akijaribu kuiomba serikali ya Kampala impe hifadhi.