Dec 21, 2018 14:38 UTC
  • Saba wauawa katika mapigano ya kikabila Ethiopia

Watu 7 wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea katika jimbo la Amhara, kaskazini mwa Ethiopia.

Naibu msimamizi mkuu wa eneo la Gonder, Bw. Bantihun Mekonen amesema, mapambano kati ya makabila ya Amhara na Qimant, yamesababisha nyumba 480 kuchomwa moto na watu wengi kupoteza makazi yao.
Mekonen pia amesema, mapigano hayo yaliyoanza tarehe 5 Desemba, yamezimwa na vikosi vya usalama vya serikali.
Qimant ni kabila la waliowachache wanaoishi katika eneo la kaskazini magharibi mwa jimbo la Amhara. Katika miaka ya hivi karibuni wanaharakati wa kabila la Qimant wamekuwa wakitaka wawe na eneo lenye mamlaka ya ndani katika jimbo la Amhara.
Hayo yanaripitiwa siku moja baada ya watu 10 kufariki dunia nchini Ethiopia baada ya kutokea mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa kando ya barabara moja magharibi mwa nchi hiyo. Vyombo vya usalama vya Ethiopia vimetangaza kuwa, mlipuko huo uliolilenga basi dogo la abiria ulitokea Jumatano.

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia anajitahidi kuleta mapatano ya kitaifa na kupunguza mapigano ya kikabila katika nchi yake 

Hivi karibuni pia watu 23 waliuawa katika machafuko yaliyozuka jirani na mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa, baada ya wafuasi wa kundi la zamani la waasi la Harakati ya Ukombozi wa Oromo (OLF) ambao wengi wao wanatoka katika kabila la Oromo, kuingia mjini Addis Ababa wakipeperusha bendera ya OLF na kupambana na wakazi wa mji huo.

Tags