Watu 16 wapoteza maisha katika hujuma ya kigaidi Mogadishu, Somalia
Watu 16 wamepoteza maisha kufuatia hujuma ya kigaidi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Taarifa zinasema gari lililokuwa limesheheni mabomu liliripuka katika kituo cha upekuzi wa jeshi karibu na ikulu ya Rais wa Somalia na kuuwa watu 16 huku wengine 20 wakijeruhiwa. Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab amedai kuhusika na hujuma hiyo.
Kati ya walipoteza maisha ni waandishi habari watatu wa televisheni ya Kisomali ya Universal TV yenye makao yake London na miongoni mwao alikuwemo mwandishi mashuhuri Awil Dahri.
Maafisa wa usalama wanasema magaidi walilenga kituo hicho cha upekuzi kilicho karibu na mlango mkuu wa ikulu ya rais wa Somalia ambayo ina ulinzi mkali.

Kundi la kigaidi la Al Shabab lilianza hujuma zake nchini Somalia mwaka 2007 na limekuwa likiendesha ugaidi katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya Somalia na pia katika nchi jirani ya Kenya. Magaidi hao walitumuliwa Mogadishu Agosti 2011 katika operesheni iliyofanywa vikosi vya kulinda amani ya Umoja wa Afrika, AMISOM, lakini wamekuwa wakifanya mashamabulizi ya kuvizia mara kwa mara.
AMISOM ina askari wapatao 21,000 nchini Somalia ambao wanalinda amani katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vya ndani kwa robo karne sasa.