Askari polisi 10 waviziwa na kuuawa kaskazini mwa Burkina Faso
(last modified Fri, 28 Dec 2018 15:57:11 GMT )
Dec 28, 2018 15:57 UTC
  • Askari polisi 10 waviziwa na kuuawa kaskazini mwa Burkina Faso

Maafisa 10 wa polisi ya Burkina Faso wameuawa katika hujuma dhidi yao katika eneo la Toeni, kaskazini magharibi mwa nchi karibu na mpaka wa Mali.

Waziri wa Usalama wa Burkina Faso, Clement Sawadogo sanjari na kuthibitisha idadi ya polisi waliouawa, amesema wengine watatu wamejeruhiwa; na kwamba msafara wa magari yao uliviziwa na kushambuliwa katika eneo la Toeni jana Alkhamisi, ukitokea eneo la Dedougou.

Mashuhuda wanasema gari lililokuwa mbele katika msafara huo lilikanyaga bomu la kutegwa ardhini na kuripuka, na hapo ndipo wavamizi waliyazingira magari mengine na kuwamiminia risasi maafisa hao wa polisi. 

Visa vya maafisa usalama kuuawa katika mashambulizi ya watu wenye kubeba silaha vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara nchini Burkina Faso. Septemba mwaka huu, askari wanane wa jeshi la nchi hiyo walipoteza maisha kufuatia mripuko wa bomu katika mji wa Baraboule mkoani Soum, mwezi mmoja baada ya maafisa usalama wengine saba kuuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini, mashariki mwa nchi.

Majeneza ya maafisa usalama wa Burkina Faso waliouawa miezi michache iliyopita

Kadhalika mwezi Mei mwaka huu, watu wenye silaha walifanya shambulizi katika mji wa Boulekessi ambao uko karibu na mpaka wa Burkina Faso na Mali, na kuua raia 12.

Makundi ya wanamgambo wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda ndiyo yamekuwa yakituhumiwa kuhusika na hujuma hizo nchini Burkina Faso.