Jan 06, 2019 08:20 UTC
  • Chama cha Madaktari Kenya: Madaktari wa Cuba hawajafuzu

Chama cha Madaktari nchini Kenya KMA kimetilia shaka uzoefu na uwezo wa kitaaluma wa madaktari wa Cuba walioenda nchini humo mwaka jana.

Rais wa chama hicho Jacqueline Kitulu amesema "Baraza Kuu la chama katika wiki chache zijazo litaandaa muswada wa sheria ya kutathminiwa tajiriba na vyeti vya masomo vya madaktari hao, ambao wanahatarisha maisha ya Wakenya."

Naye Naibu Rais wa chama hicho cha Kenya Medical Association, Lukoye Atwoli amesema, "Hatujui chochote kuhusu kufuzu kwao katika taaluma hii, kwa msingi huo hatuwezi kusema iwapo ni wataalamu wa tiba au la."

Mwezi Mei mwaka uliomalizika wa 2018, madaktari zaidi ya 100 kutoka Cuba waliwasili Kenya na kutumwa katika kaunti zote 47 kupiga jeki sekta ya afya nchini humo.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipokutana na Rais wa wakati huo wa Cuba, Raul Castro

Aidha madaktari wapatao 50 kutoka Kenya walielekea Cuba mwezi Septemba kwa ajili ya mafunzo ya miaka miwili.

Katika safari ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya nchini Cuba mwaka jana, alifanya mazungumzo na rais wa nchi hiyo wakati huo, Raul Castro, ambapo nchi mbili zilitliana saini mikataba ya ushirikiano katika sekta za afya.

Tags