Feb 05, 2019 16:00 UTC
  • Nchi za Magharibi ikiwemo Marekani zaiomba radhi Afrika Kusini

Balozi za nchi tano za Magharibi nchini Afrika Kusini zimemuandikia barua ya kuomba radhi Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo, baada ya kukiuka protokali za kibalozi.

Nchi hizo zimekiri katika barua hiyo kwa Ramaphosa kuwa ni kweli zilikiuka taratibu za diplomasia.

Barua ya mabalozi hao wa Marekani, Uingereza, Ujerumani, Uswisi na Uholanzi ilimuonya Rais Ramaphosa kwamba vitega uchumi vya wageni viko hatarini, iwapo hatakaza kamba katika vita dhidi ya ufisadi.

Serikali ya Afrika Kusini hapo jana ilielezea kusikitishwa kwake baada ya Marekani na balozi nyingine za Ulaya kumuandikia barua hiyo Rais Cyril Ramaphosa zikimtaka achukue hatua zaidi za kupambana na rushwa na kuimarisha mazingira mazuri ya biashara kwa wawekezaji.

Ramaphosa na mtangulizi wake Jacob Zuma anayeandamwa na tuhuma za ufisadi

Waziri wa Mambo ya  Nje wa Afrika Kusini amesema mabalozi wa Marekani na nchi hizo za Ulaya wamevunja protokali kwa kuilalamikia moja kwa moja Ofisi ya Rais. Chama tawala cha ANC kimezitaja nchi hizo zilizomuandikia barua Ramaphosa kama mabeberu ajinabi.

Aidha Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini (DIRCO) imesema onyo hilo la nchi tano za Magharibi kwa Afrika Kusini ni ishara ya kuporomoka kwa misingi ya diplomasia.

Tags