Baada ya mgomo, sasa walimu Tunisia wafanya maandamano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51394-baada_ya_mgomo_sasa_walimu_tunisia_wafanya_maandamano
Maelfu ya walimu nchini Tunisia wamemiminika mabarabarani katika mji mkuu Tunis kushiriki maandamano yaliyoitishwa kwa lengo la kuishinikiza serikali iliyokataa kuwapandishia mishahara wafanyakazi wa umma.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2019 11:10 UTC
  • Baada ya mgomo, sasa walimu Tunisia wafanya maandamano

Maelfu ya walimu nchini Tunisia wamemiminika mabarabarani katika mji mkuu Tunis kushiriki maandamano yaliyoitishwa kwa lengo la kuishinikiza serikali iliyokataa kuwapandishia mishahara wafanyakazi wa umma.

Walimu hao ambao wamekuwa katika mgomo tokeo mwezi Oktoba mwaka uliopita 2018 wameshiriki maandamano hayo kuitikia mwito uliotolewa na muungano wenye nguvu wa wafanyakazi nchini humo UGTT.

Walimu hao wamemtaka Waziri wa Elimu, Hatem Ben Salem ajiuzulu wakisisitiza kuwa yeye ndiye kizingiti katika mchakato wa kufikiwa malengo yao.

Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na jumbe zinazosema, "Ondoka" na "Suluhisho ni kujiuzulu".

Maandamano ya huko nyuma ya watumishi wa serikali mjini Tunis

Maandamano hayo ya walimu yamefanyika wiki mbili kabla ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kushuhudia mgomo wa nchi nzima wa sekta ya umma, unaotazamiwa kufanyika Februari 20 na 21.

Muungano mkubwa zaidi wa kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini Tunisia UGTT umetoa mwito wa kufanyika mgomo huo wa nchi nzima ili kushinikiza kupandishwa mishahara ya wafanyakazi laki sita na sabiini elfu (670,000) wa sekta ya umma.