Kesi ya kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu Tanzania yaanza kusikilizwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51397-kesi_ya_kupinga_uteuzi_wa_mwanasheria_mkuu_tanzania_yaanza_kusikilizwa
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam nchini Tanzania imeanza kusikiliza kesi ya kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi uliofanywa na Rais John Magufuli tarehe Mosi Februari mwaka jana 2018.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2019 11:17 UTC
  • Kesi ya kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu Tanzania yaanza kusikilizwa

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam nchini Tanzania imeanza kusikiliza kesi ya kupinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi uliofanywa na Rais John Magufuli tarehe Mosi Februari mwaka jana 2018.

Fatma Karume, Wakili na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) anaongoza mawakili wenzake upande wa mashtaka kupinga uteuzi huo.

Ado Shaibu, Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT -Wazalendo ndiye aliyefungua madai hayo ambayo yameanza kusikilizwa leo tarehe 7 Februari mwaka 2019.

Madai hayo yamefunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo Ado anapinga utaratibu uliotumika kuteuliwa Dk. Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakili Fatma Karume

Kwenye kesi hiyo namba 29 ya mwaka 2019 Ado ameiomba mahakama mambo matatu: Mahakama itamke kuwa Rais Magufuli amevunja Katiba kwa kumteua Dk Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu, mahakama itamke kuwa Dk. Kilangi amevunja Katiba kwa kukubali kuteuliwa na Rais Magufuli kinyume na Katiba na pia mahakama itamke kuwa uteuzi huo sio halili na ni uvunjifu wa Katiba ya Nchi.

Mahakama imeipa serikali siku 14 kujibu mashtaka ya Ado. Shauri hilo limeahirishwa mpaka tarehe 22 Februari mwaka huu kwa ajili ya kusikiliza majibu ya serikali juu ya mashtaka hayo.