Lowassa atangaza kurejea CCM, Tanzania, Sumaye asema hakushangaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51880-lowassa_atangaza_kurejea_ccm_tanzania_sumaye_asema_hakushangaa
Waziri Mkuu wa zamani nchini Tanzania ambaye alikuwa mgombea urais kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Edward Ngoyai Lowassa leo ametangaza uamuzi wa kuhama chama hicho na kurejea chama tawala (CCM).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2019 12:50 UTC
  • Lowassa atangaza kurejea CCM, Tanzania, Sumaye asema hakushangaa

Waziri Mkuu wa zamani nchini Tanzania ambaye alikuwa mgombea urais kupitia tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Edward Ngoyai Lowassa leo ametangaza uamuzi wa kuhama chama hicho na kurejea chama tawala (CCM).

Lowassa amerejea ndani ya chama chake cha zamani katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam ambapo amepokelewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania. Hatua ya waziri mkuu huyo wa zamani kurejea chama tawala CCM ameichukua ikiwa ni baada ya kupita miaka mitatu tangu alipotangaza kukihama chama hicho na kujiunga na chama cha upinzani cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA hapo tarehe 28 Julai 2015 baada ya jina lake kukatwa katika mchujo wa wagombea urais wa CCM mwaka huo. Katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni chama cha CHADEMA kimeshuhudia wimbi la wabunge na makada wake kuhamia chama tawala kwa madai ya kuunga mkono shughuli za maendeleo za Rais John Magufuli.

Siku ambayo Edward Ngoyai Lowassa alipochukua fomu kugombea urais Tanzania 2015

Kufuatia hatua hiyo Frederick Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani amesema kuwa, uamuzi uliochukuliwa na Edward Lowassa kurejea Chama cha Mapinduzi (CCM) hauwezi kumshtua hata kidogo. Akizungumza muda mfupi baada ya Lowassa kutangaza hatua yake hiyo, Sumaye amesema: "Mimi hainipi shida, mtu akiamua kuhama chama na kwenda kingine ni uamuzi wake.” Amesema. Akijibu swali aliloulizwa  iwapo na yeye ana nia ya kuondoka upinzani na kurejea CCM amesema: "Kama kaamua acha aende, sisi tutaendelea kujenga chama na hicho unachokisema cha kuhama ni ndoto ambayo haipo.”